2 research outputs found

    Thamani ya Ujumi wa Kiafrika katika Hadithi Fupi Simulizi za Kiswahili

    Get PDF
    Kuibuka kwa mijadala kuhusu ujumi wa Kiafrika katika nyuga mbalimbali ukiwamo uga wa fasihi, kumechangiwa na mahusiano ya kihistoria ya Waafrika na watu wa mataifa mengine, hususani watu kutoka jamii za Kimagharibi. Kwa karne nyingi Waafrika wameonekana ni jamii ya watu duni, washenzi, washirikina na kwamba Afrika hakuna chochote chenye maana wala chenye kuvutia (Neugebauer, 1991). Mitazamo ya namna hiyo katika kutathmini ulimwengu wa Kiafrika haijaishia kwa wageni tu, bali hata baadhi ya Waafrika walioathiriwa na elimu ya Kimagharibi huuzungumzia utamaduni wa Kiafrika na fasihi yake kwa namna hiyohiyo. Hili linadhihirika bayana pale tunapoona fasihi simulizi ya Kiafrika ikiwamo fasihi simulizi ya Kiswahili inapigwa kumbo na Waafrika wenyewe katika maeneo mbalimbali muhimu ya kijamii (Sanga, 2018). Makala haya yamechambua hadithi fupi simulizi kama sehemu ya fasihi simulizi ya Kiswahili ili kuonesha thamani za ujumi wa Kiafrika kwa ustawi wa jamii za Kiafrika. Utafiti uliozalisha makala haya ulikuwa wa kimaktaba na uwandani. Aidha, data zilikusanywa kwa kutumia mbinu za uchanganuzi matini na mahojiano. Utafiti ulitumia mkabala wa kitaamuli katika uchambuzi na uwasilishaji wa data. Aidha, data hizo pia zilichanganuliwa kwa kutumia misingi ya Nadharia ya Ujumi Mweusi

    Athari za Mkengeuko wa Ujumi wa Kiafrika katika Hadithi Fupi Andishi za Kiswahili

    No full text
    Mkengeuko wa ujumi katika uga wa fasihi hurejelea hali ama ya mwandishi au msomaji kutovutiwa kuandika au kusoma kazi  zinazohusu maisha halisi ya tabaka lake au utamaduni wa jamii yake. Badala yake hugeuka na kuvutiwa kuandika au kuzisoma kazi za fasihi za tabaka au jamii zenye utamaduni usioelekeana na wake (Sanga, 2018). Katika makala hii zimechunguzwa baadhi ya hadithi fupi andishi kutoka katika magazeti ya HabariLeo, Nipashe na Mwananchi ya mwaka 2008 hadi 2014, ambazo ni sehemu ya kipindi cha utandawazi. Hadithi fupi andishi za Kiswahili za kipindi hiki cha utandawazi, zimekengeuka kiujumi kutoka kwenye zile za asili ambazo ni hadithi fupi simulizi. Ukengeufu umejikita katika namna hadithi zinavyotungwa, zinavyohifadhiwa, zinavyoifikia hadhira, masuala yanayojadiliwa, mahali na wakati wa kusomwa. Hali hiyo imeufanya utanzu huu kuwa na sifa zinazokaribiana na riwaya kiasi cha  kupoteza utambulisho wake. Aidha, hadithi fupi za sasa zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na usasa pamoja na umiji, jambo lililosababisha utanzu huu kuibagua hadhira, kirika na kimaeneo. Vilevile, maudhui ya hadithi fupi andishi yameonekana kuwa na mvuto kwa vijana wa mjini kuliko wazee. Hii ni kwa sababu visa vyake vingi na matukio huhusu mapenzi ya kisasa, masuala ya uhalifu, ugaidi na maisha ya  wanafunzi wa vyuo vikuu. Matukio haya yanawagusa zaidi vijana kuliko wazee. Jamii za sasa za Kiafrika zimekengeuka kiujumi na kuvutiwa na mambo yanayofungamana na utamaduni wa Kimagharibi kuliko wa Kiafrika
    corecore