Lengo la utafiti huu kama lilivyobainishwa katika sura ya kwanza ilikuwa ni
kuchunguza dhima ya vipengele vya kimtindo katika tamthiliya za kihistoria kwa
kulinganisha tamthiliya ya Morani na Kinjeketile ili kubaini vipengele
vinavyowafananisha na kuwatofautisha wasanii wa vitabu hivyo katika kuliwasilisha
suala la kihistoria. Utafiti huu ulitumia mbinu tatu za ukusanyaji data ambazo ni;
maktaba, usaili na dodoso. Sampuli iliteuliwa kwa kutumia mbinu ya madhumuni
maalumu na uteuzi rahisi. Aidha data za utafiti huu zilichambuliwa kwa kutumia
mbinu ya uchambuzi maudhui na uchambuzi linganishi. Utafiti huu uliongozwa na
Nadharia ya Elimumitindo katika Uchambuzi wa Matini za Kifasihi. Utafiti
umegundua kuwa, tamthiliya hizi zinatofautiana katika mbinu za kisanii na ubunifu.
Tamthiliya ya Morani imetumia mbinu na lugha ya kitamathali wakati tamthiliya ya
Kinjeketile imetumia lugha ya kawaida, rahisi na ya wazi zaidi. Aidha utafiti huu
umebaini kuwa, tamthiliya hizi zinatofutiana katika kuwasilisha suala la kihistoria
kwa sababu wasanii wanawasilisha historia ya jamii ya Tanzania katika vipindi
viwili tofauti. Morani anawasilisha historia katika kipindi cha baada ya uhuru na
hivyo kujadili juu ya historia ya harakati za kupambana na ukoloni mamboleo wakati
Kinjeketile inajadili kwa uhalisia juu ya harakati za jamii za kusini katika kupambana
na ukoloni mkongwe, yaani, ukoloni katika utawala wa Mjerumani. Kwa upande
mwingine, ilibainika kuwa tamthiliya hizi kwa vile zimeandikwa na wasanii wa jamii
moja ambao wameshuhudia na kupata masimulizi ya historia ya jamii yao. Wasanii
hawa wanafanana katika kuwasilisha maudhui ya kazi zao ambapo wote kwa pamoja
wanajadili juu ya mambo mbalimbali yaliyopo katika jamii kama vile; rushwa,
harakati za ukombozi, usaliti, unyonyaji na ukandamizaji